Wednesday, November 30, 2011

Ninakunywa nisahau

Ninakunywa nimsahau, mpenzi wangu wa zamani,
Tanzania ya nahau, upendo na ulaini,
Aliyekuwa mdau, mwandani mwenye imani,
Ninakunywa nisahau, masahibu nchi yangu!

Amenifanya bahau, tena hatuaminiani,
KIsha ananidharau, na kuwapenda wageni,
Nikijaribu msahau, ninashindwa kwa yakini,
Ninakunywa nisahau, masahibu nchi yangu!

Anitenda makuruhu, ila yungali moyoni,
Yamenishinda malau, nataka hama nyumbani,
Nachelea kuwa mwehu, kumuacha mawazoni,
Ninakunywa nisahau, masahibu nchi yangu!

Namuomba Binti Chau, akienda redioni,
Ushauri kunukuu, Hamada niuthamini,
Siridhiki na makuu, mlevi nifanye nini?
Ninakunywa nisahau, masahibu nchi yangu!

Zimenitoka nahau, mwenzenu majaribuni,
Sasa ni mifupa na fuu, nyama sinayo mwilini,
Na mwingi wa kusahau, nami si usingizini,
Ninakunywa nisahau, masahibu nchi yangu!

No comments: