Sunday, November 13, 2011

Twajaribu, twathubutu

Huwezi kunchezea, na akili nimepewa,
Zezeta wanidhania, kama ndivyo wapotea,
Na leo utanijua, mshairi napangua,
Twajaribu, twathubutu, wanafiki nawaita!

Ninapangua hadaa, umma mnaofanyai,
Ukweli mnaujua, mwatudhania vichaa,
Nyie mliokwishakuwa, na hao mnaowafaa,
Twajaribu, twathubutu, uongo kuutengeza!

Baba tulimshangaa, uoza kuukataa,
Nao mbolea wafaa, rushwa kuja kulea,
Na dini kuitumia, dekio la kudekia,
Twajaribu, twathubutu, uoza kuutumia!

Vibaya tunavitumia, vyombo tulivyojaliwa,
Miaka yagereshea, harusi mtaingia,
Toboa tobo toboa, asiyejua kujua,
Twajaribu, twathubutu, taifa kulihadaa!

Nchi tumeipindua, bada kufa ujamaa,
Kila kitu twachukua, hata visivyotufaa,
Mali ya umma ruia, ndoto haikutimia,
Twajaribu, twathubutu, shamba la bibi kuvuna!

Baada ya kunyakua, wengine twawaachia,
Wawekezaji radhia, wabia wa kuchagua,
Ambao wanatufaa, sisi na zetu jamaa,
Twajaribu, twathubutu, ujamaa kifamilia!

Hakuna kumchagua, kiongozi wa kufaa,
Ikiwa anatokea, chama chetu asokua,
NI heri kushupaa, dungayembe kuchagua,
Twajaribu, twathubutu, ukabila wa kichama!

Na ndugu kuzingatia, ndio wanaotufaa,
Hao wengi twachagua, wenyewe kujiwekezea,
Kesho ikijafikia, watajatusaidia,
Twajaribu, twathubutu, udugu kujifanyia!

Wazee twawatania, maslahi kupalilia,
Kumbe twajivunia,cha kwao kukichukua,
Kisha kuwasingizia,walikwishakukichukua,
Twajaribu, twathubutu, wazee kuwahadaa!

Kinamama 'bati' mbaya, ujinga wamejaliwa,
Vigelegele kukodiwa, kisha ubunge wapewqa,
Abyadhi walokua, kichwani zilishapaa,
Twajaribu, twathubutu, kinamama kununua!

Vijana wanadhania, watajakusaidiwa,
Debe kutupigia, ni kazi walojialiwa,
Mengine hatujajua, kwanini wazungumzia,
Twajaribu, twathubutu, vijana kuwahadaa!

Ni wazito kuelewa, mchezo hawajaujua,
Rahidi wanadhania, nchi kuisimamia,
Eti bila kukwapua, na hazina kufagia,
Twajaribu, twathubutu, vijana kuwahadaa!

Raia ng'ombe wa maziwa, twapaswa kumkamua,
Nini mnaulizia, na hili mnalijua,
Mbadala upi mwajua, tupeni tutautumia?
Twajaribu, twathubutu, kumkama Mtanzania!

Mishahara twalilia, haki yetu imekua,
Na posho kuongezewa, hata nchi ikiwa na njaa,
Wachache tulochaguliwa,pepo yetu ni dunia,
Twajaribu, twathubutu, kujilipa kitajiri!

Magari hatutakataa, sisi sio makataa,
Heshima tutajivunia, vipi bila nayo kua,
Bure mwatusimbulia, ni wivu nyie mwajaa,
Twajaribu, twathubutu, magari yetu ya fahari!

Ufisadi ni kujua, kipi hakijatumiwa,
Na sisi kukitumia, ndugu zetu na jamaa,
Hicho tulishaamua, macho mnang'aa ng'aa!
Twajaribu, twathubutu, ufisadi tumeweza!

Rada tulishainunua, mbovu sana ilokuwa,
Majira walifichua, waongo wakaambiwa,
Miaka imeshagundua, kumbe kweli ilikuwa?
Twajaribu, twathubutu, rada mbovu kununua!

Zanzbar kuingia, dhuluma tukanuia,
Kura kuwaibia, kushinda waliokuwa,
Wakabaki walialia, hawajui kinachotokea,
Twajaribu, twathubutu, hata kura kuziiba!

Ni mradi wa manufaa, chama kinaendelea,
Hamsini ilikuwa, sasa mia kutimia,
Wajinga kazi kuliwa, au hili mwalikataa?
Twajaribu, twathubutu, hata kura kuziiba!

Magari tukinunua, bei mbaya twachagua,
Ukubwa sio izaya, na wala haujawa jaa,
Vizuri kuvichagua, inda, tadi zawajaa?
Twajaribu, twathubutu, magari yetu ya fahari!

Shule tunawambia, wanafunzi wamezoea,
Viatu kutokuvaa, na viti kuvitumia,
Madawati yawasumbua, yanini kuwapelekea?
Twajaribu, twathubutu, shule bila madawati!

Imeshaingia asilia, tiba inayotufaa,
Yanini kuweka dawa, ni nani atatumia,
Babu azidi vumbua, nyingine zinazofaa,
Twajaribu, twathubutu, zahanati bila dawa!

Wahandisi wazubaa, kutengeza hawajua,
Trekta la Kitanzania, mazingira kuyavaa,
Tuachaje kununua, na pasenti kupatia?
Twajaribu, twathubutu, kilimo pasi trekta!

Udugu tumeingia, na Angulo wa Ulaya,
Marekani nao pia, bure tunawauzia,
Dhahabu kuichukua, sisi mashimo yafaa,
Twajaribu, twathubutu, kugawa dhahadu yetu!

Sisi mashimo yafaa, kuweka maji ya mvua,
Takataka kutupia, na kokoto kuzikwaa,
Ni mzungu na mwasia, madini wanaojua,
Twajaribu, twathubutu, kurejesha ombaomba!

KIsiwani tumekaa, hatuji ya dunia,
Mathalani Korea, pia nako Malaysia,
Kadhalika na India, nao Brazil pia,
Twajaribu, twathubutu, kutokuiga ya China!

No comments: