Thursday, November 10, 2011

Walopewa wake wema

Waliopewa wake wema, huwafanza maadui,
Elewa muacha pema, pabaya patamstahi,
Maisha huja kukwama,pale usipotanabahi,
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

Waliopewa wake wema, bahati hawatambuia,
Hugeuka ni wanyama, wakawatoa nishai,
Maisha ni uhasama, hakuna la kujidai,
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

Huukataa uzima, mauti kuyasabahi,
Hujivunjia heshima, ndani na mwenye jinai,
Hata kama ni ulama, ni heri ya ndugu mui,
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

Waliopewa wake wema, neema hawaijui,
Maziwa wenda kukama, ya mbwa mwitu na chui,
Meli ikenda mrama, dhiki hoi bin hoi,
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

Penye miti ni nakama, wajenzi hawakai,
Na kama chombo kugema, mafundi hujakinai,
Kwenye maji huja zama, kwa vifo si majeruhi,
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

Dunia hii daima, yakini inajirai,
Iweje wenye hekima, taahira kujidai,
Walojaa uadhama, kuwa ni matandabui?
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

Asili sijaifuma, kusikia sijawahi,
Ni siri yenye alama, ambayo siitambui,
Naisubiri rehema, kubainishwa wahyi,
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

Kweli wenye wake wema, huwa hawalitambui,
Hawajui walochuma, washindwa kukistahi,
Naghairi maamuma, watu hao kuwarai,
Walopewa wake wema, sikuzote hawajui!

No comments: