Wednesday, November 30, 2011

Shule haina elimu

Hapa si mastakimu, inafaa kutambua,
Watu wasio adhimu, vingine hupadhania,
Wakajitia muhimu, daima kujizuzua,
Shule haina elimu, nani ataisomesha?

Na nilipotakadamu, hili nikaligundua,
Shule haina elimu, nani ataipatia,
Haipo yake kasimu, nani kuyagharamia,
Shule haina elimu, nani ataisomesha?

Ujinga kweli ni sumu, na wengi inshawaua,
Wengi wanajituhumu, badala ya kutuhumiwa,
Ubongo bila ya damu, muhali kufikiria,
Shule haina elimu, nani ataisomesha?

Wachache wanaofahamu, ni wengi wasiojua,
Na mengi kwetu haramu, ila tunayatumia,
Ni muhali wa kukimu, adhana isipokua,
Shule haina elimu, nani ataisomesha?

Niliwauliza wa Lamu, Fumo Lyongo akiwa,
Wanipe zao salamu, ufumbuzi kuujua,
Hawajaenda Kiamu, jibu hawajalitua,
Shule haina elimu, nani ataisomesha?

No comments: