Sunday, November 27, 2011

Nishani kwa mwalimu?

Huwa hana wadhifa, anzia na kitaifa,
Ukija kimataifa, hayo ya mbali masafa,
Labda wampe FIFA, kazi ya soka urefa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Mwalimu fakiri hufa, hii ndiyo yake sifa,
Akiwapa maarifa, wajao jenga ghorofa,
Malapa ni yake sifa, nyumba yake ina ufa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Mshaharawe maafa, na kukopwa yake dhifa,
Hata akiwachachafya, hali mkate wa mofa,
Hubakia kuwa lofa, bila mapya maarifa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Huwa naipiga chafya, kwa elimu taarifa,
Iwe bora kitaifa, wakati zazidi nyufa,
Walimu kwenye maafa, wakuze vipi wadhifa?
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Itabakia kifafa, elimu ya kitaifa,
Nusura sio sharifa, katika haya masafa,
Kwa Wachaga na Waswafa, tunatakiwa hanifa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Iwe ya kimataifa, kwa maudhui na sifa,
Na lugha iwe wadhifa, Kiswahili maarifa,
Lugha ziwe falsafa, kusomwa hadi yakufa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Lugha ziwe falsafa, kusomwa hadi yakufa,
Chekechea makhalifa, mwanzo waijenge sifa,
Vyuoni iwe tarafa, za wageni swahifa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Maudhui si kashfa, kwa Kiswahili latifa,
Wachina kwa maarifa, ndivyo wanavyosahifa,
Lugha ngeni taarifa, kuongezea wadhifa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

Atujalie Raufa, tujezipanda ghorofa,
Elimu na maarifa, visijekosa wadhifa,
Tulinyanyue taifa, liwe la kimataifa,
Mwalimu bora ni nani, shindano kimataifa?

No comments: