Sunday, November 13, 2011

Tukumbushane wajibu

Kila mtu amepewa, na katiba na sheria,
Haki zilizokubaliwa, na anapaswa kujua,
Kuzichunga kwa hatua, na kwingine kutetea,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

Mabwana wanaokua, kweli kuwatengenea,
Walipo wakajijua, uumba hawajaupewa,
BInadamu wabakia, na twaweza kuwatoa,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

Visheni kufafanua, na njia kuiandaa,
Nayo tutaitumia, malengo kuyafikia,
Wote wamoja tukiwa, bila baa na balaa,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

Misheni kuiamua, nini tunatarajia,
Sisi tuliokwishazaliwa, na watakaotufuatia,
Ili wasije kupotea, kizazi kutokomea,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

Viongozi wanaokua, nafasi kuzitambua,
Masultani hawajawa, wao na vizazi vyao pia,
Ukiritimba nazaa, waache kuendelea,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

Vijiji kuviokoa, sasa vinaangamia,
Maendeleo afua, huenda yakatokea,
Visiwe vinazubaa, dunia yatangulia,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

Vijana wanapotea, nani wa kuwaongoa,
Kiongozi angekuwa, jeshi angelitumia,
Mapinduzi kuja zua, nasi kuyafagilia,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

Tusikubali raia, kuburuzwa na wanaa,
Ukweli kuwaambia, na hatua kuchukua,
Vingine kupigania, haki tukaikomboa,
Tukumbushane wajibu, uhuru na haki zetu!

No comments: