Sunday, November 13, 2011

Kukumbushana

'Sichoke kukumbushia, viumbe tumeamriwa,
Kurudi na kurudia, iwe ni yetu tabia,
Na walioachaguliwa, huja wakaokolewa,
Kukumbushana ni kheri, wapo wanaosikia.

Dunia inapotea, sisi tunaiangalia,
Uchunga kubadhiwa, mashakani twajitia,
Na kwake tutarejea, utetezi bila kua,
Kukumbushana ni kheri, wapo wanaosikia.

Hata wakubwa wakiwa, ukweli kuwaambia,
Na wakishausikia, wenyewe wataamua,
Kazi yako huishia, hapo ulipofikia,
Kukumbushana ni kheri, wapo wanaosikia.

Ufisadi waenea, na watu kudhulumiwa,
Haki inanunuliwa, na uhuru wazuiwa,
Kila ukiangalia, hakuna wa kukemea,
Kukumbushana ni kheri, wapo wanaosikia.

Kukumbushana usia, sisi tumeupokea,
Tukifanyia mzaha, sote tutaangamia,
Na kwa huruma Alaa, katu hatatuagalia,
Kukumbushana ni kheri, wapo wanaosikia.

No comments: