Tuesday, November 15, 2011

Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

IKIWA bado mwalala, mwahitajika vijana,
Mapinduzi yanakua, kwa usiku na mchana,
Marekani kuanzia, Ulaya sasa kwa sana,
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

Viongozi twaonea, hawana wanalo sana,
Wao pia watumiwa, na mabepari wenye zana,
Makampuni ya dunia, ndiyo yanayotubana,
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

Salamu mnatumiwa, changamkeni vijana,
Kuamka mwatakiwa, msifanze danadana,
Ni hatia kuchelewa, ntasgubdwa kuungana,
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

Sitini yaliyotokea, wakashindwa ongozana,
Mfumo ukaendelea, hadi leo wasutana,
Sasa kinachotakiwa, kiongozi wa amana,
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

Mabepari wa dunia, wao wameshaungana,
Wanazikwapua hazina, masikini twabakia,
Vibarakala watwana, nao wanawatumikia,
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

Uwakilishi wavia, weshafanywa ni watwana,
Matumbo watumikia, sio wenu muamana,
Wenyewe msipojitoa, mtajaumizwa sana,
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

Yaandamana dunia, ubepari wachukia,
Wazidi nuka hadaa, na kuvuja kwa usaha,
Ni ipo sasa nasaha, vijana watasikia?
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

Hatima sijaijua, ila sianzi paua,
Ukuta sijanyanyua, sijui kama ntakaa,
Nayangoja majaliwa, kujua sikujaliwa,
Wahitajika vijana, mapinduzi ya dunia.

No comments: