Aja kuwatumia, wajinga waso hamasa,
Hiyo ni yake tabia, yeyote mwanasiasa,
KIla akikusalimia, ni kura anapepesa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Ni wengi huwatumia, mfano kwake asusa,
Au muwa unavyoliwa, tena kwa kutomasatomasa,
Kisha likatupwa bua, hata mbwa kutonusa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Wasomi huwatumia, wakaona wanaposwa,
Waandishi nao pia, hukumbwa nacho kisa,
Na wote wasiojua, kwake yeye ni darasa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Wanavijiji walia, hawana linalopasa,
Wanaowatumainia, wamefanyia mkasa,
Nyuma wananing'inia, kila mtu kawasusa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Walimu wanababia, wakishapigwa msasa,
Ila alowagutua, ghorofa wameibarasa,
Kwani walishajua, muongo mwanasiasa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Madaktari watamia, wadhani hawajaguswa,
Lakini ninavyojua, India kwenda ndio kisa,
Waonekana nazaa, wakubwa kuwapapasa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Uhuni walivyojaa, mapadri huwatosa,
Mashehe wasingiziwa, madawa wanadodosa,
Doa ndoa imeingia, hivi sasa kisa na mkasa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Hili hawajalijua, mapolisi wananesa,
Misri hawajaijua, wala bado kuinusa,
Ila yajanayo ingia, kwa gia yenye hamasa,
Ajua kuwatumia, wajinga mwanasiasa!
Tuesday, November 8, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment