Wednesday, November 30, 2011

Darasa halidurusi

Darasa letu nuhusi, mambo yake w asiwasi,
Kalivaa ibilisi, kila kitu ni yabisi,
Maneno kama kamasi, na mafua ya utosi,
Darasa halidurusi, fikra zina nakisi!

Darasa Abunuwasi, mapya haliasisi,
Limejaa ubinafsi, ya umma kwao mkosi,
Wote wake waasisi, dhehebu wameliasi,
Darasa halidurusi, fikra zina nakisi!

Kawajaa ibilisi, dahari watanafusi,
Hawataki ufuasi, wa mauti kuwahisi,
Wataka ishi fususi, iwe radhi ya Qudusi,
Darasa halidurusi, fikra zina nakisi!

Awadanganya muasi, atawavisha libasi,
Iwe kwao majilisi, dunia isiwatusi,
Waishi yao kiasi, kiongozi ibiisi,
Darasa halidurusi, fikra zina nakisi!

Naona kuna nakisi, na hili wanalifosi,
Hajatokea msusi, hili akaja liasi,
Kufa kwetu mahsusi, kuishi si yetu chunusi,
Darasa halidurusi, fikra zina nakisi!

Nakiondoa kifusi, msiwe na wasiwasi,
Maisha si almasi, ardhi kuwa damisi,
Iishi bila anasi, milele ikatulia,
Darasa halidurusi, fikra zina nakisi!

No comments: