Wednesday, November 30, 2011

Kituo cha afya hoi

Kituo kiko taabani, homa inakisumbua,
Daktari wake nani, aje kukiangalia,
Nyuzize ni hamsini, joto limeparamia,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Malaria yumkini, maradhi tunahofia,
Isije enda kichwani, mgonjwa awe kichaa,
Tutakuwa mashakani, akianza kukimbia,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Nesi hawaaminiani, ni nani wa kumwambia,
Kuuliza wa zamu nani, daktari alokua,
Mgonjwa kumuauni, nafuu akaijua,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Majibu yao utani, na mengine ni mzaha,
Fakiri hawajioni, mzuri hawajamjua,
Kila mtu hatiani, ubaya wameshamtia,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Mlinzi usingizini, kazi mbili kazidiiwa,
Usiku yuko lindoni, mchana getini atua,
Kumwamsha kabaini, kituo kimevamiwa,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Kutugungua wageni, ndipo alipotulia,
Kumhoji kwa yakini, ulozi kahadithia,
Kimelogwa kwa yakini, na majirani wabaya,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Ramli keshaamini, lazima kukipigia,
Ajulikane ni nani, mema asiyekitakia,
Hoja hatukuamini, kusepa tukaamua,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Tarishi katoka ndani, wote tukamrukia,
Dakatari wa zamu nani, mgonjwa amezidiwa,
Katupeleka nyumbani, daktari ana njaa,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Mlo kakosa maskini, mke kamkimbia,
Kafuata wa mjini, wajuao kuchagua,
Na kula vyenye thamani, si matembele kuzoa,
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

Maneno kwisha kinywani, haraka tukajizoa,
Tukarudi maskini, maswali twaulizia,
Hali hii yumkini, mgonjwa atatibiwa?
Kituo cha afya hoi, daktari wake nani?

No comments: