Sunday, November 13, 2011

Muundo uliochakaa

Muundo ukichakaa, uwezo hujazidiwa,
Kubeba ukakataa, hata vyepesi vilokua,
Na nati zikalegea, na bolti kuachia,
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Hiki kimeshatokea, kwa chama kilichokua,
Grisi hakikutumia, mitambo imefubaa,
Mashine zinatitia, na uwezo kupungua,
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Uzalishaji wavia, na neema haijawa,
Kasi imeshapungua, na ari kutokomea,
Kilichobaki makaa, maji yameshaingia,
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Wajanja wanatumiwa, wajinga kuja wazaa,
Viwango vimepotea,na adili yaugua,
Na kinachoendelea, mgonjwa anazidiwa,
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Leo kinachofatia, watu wanshapagawa,
Mzuri hawajamjua, na uzuri ulokuwa,
Mbaya waliyeambiwa, malaika anakua,
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Izaya zimezidia, na hadaa majaliwa,
Matapishi yatumiwa, mchuzi kujaungia,
Na kamasi imekua, siagi ya kupakaa,
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Sasa kila muelewa, pembeni aangalia,
Kila anayejisifia, toka chini kumjua,
Na kisha kuulizia, nani anayemtumia?
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Vitu vinaendelea, kwa kudra ya maridhia,
Hata mtoto angekuwa, aweza kusimamia,
Kila kitu sawa kikawa,pengine bora yakawa,
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

Na hili nimechungua, mshairi nashangaa,
Muumba kweli shujaa, na dunia ni hadaa,
Baraka waliopewa, washindwa kuitumia?
Muundo uliochakaa, hushindwa kubeba vingi.

No comments: