Monday, November 21, 2011

Birigiji

Kitamba kishachoka, imebaki mazoea,
Rangi inafutika, chazidi kufubaa,
Ukata umenishika, siwezi tena nunua,
Birigiji imechoka, njano imeshapotea!

Wale niliowashika, uchuro wanichulia,
Tayari wanshanizika, wangoja kunifukia,
Utajiri nilozika, waje kuufukua,
Birigiji imechoka, njano imeshapotea!

Miguu inachanika, magoti yanatitia,
Watu wakereheka, hawataki niangalia,
Na sasa nimeishika, dhana ya kunyanyapaa,
Birigiji imechoka, njano imeshapotea!

Ila siachi kucheka, kila nikiwaangalia,
Hukumu wanaoweka, hivi itanifikia,
Au wao kuwafika, nami nashuhudia?
Birigiji imechoka, njano imeshapotea!

Laiti ningebahatika, ukweli nikaujua,
Ni moja tu ningeshika, hadi juu nikapaa,
Ninabaki nateseka, johari sijavumbua,
Birigiji imechoka, njano imeshapotea!

Jaha haikunitaka, toka nilipozaliwa,
Kazi kushughulika, riziki kuokotea,
Zao halitaniweka, ila mwenyewe kuvua,
Birigiji imechoka, njano imeshapotea!

No comments: