Friday, November 18, 2011

Haramu na halali

NANI asiyetambua, haramu kilichokua,
Halali hakitozaa, ila kwa kubambikia,
Mwanaharamu akiwa, huachi kumgundua,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

Ndivyo dunia yajua, kinyumewe haijawa,
Haya ukifuatia, siri utaielewa,
Kila ukweli mchelea, huja yakamuumbua,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

Nadhiri sintoitoa, nikaja kujeruhiwa,
Nitokako sijajua, kilichokwishakutokea,
Na mwenye kujua haya, ni pekee adilia,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

Waweza kushupalia, uhalali kuulilia,
Hata ndani kuingia, sebuleni kutulia,
Bado utajafulia, chenyewe kukuumbua,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

Uongo utauzaa, na kisha kuulea,
Kisomo kukipatia, na daawa mashalaa,
Ila chako kisokuwa, hakitakuja kukurudia,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

Nasaba ina ulua, na sumaku yavutia,
Hazipishani tabia, na mwenendo hufatia,
Walo nje hutambua, chako na kisichokua,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

Ya mwongo ni fupi njia, na matuta yamejaa,
Na usipoangalia, meno waweza ng'olewa,
Na chini waliokaa, hujikuta wanaelea,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

Siri sintoifichua, uyusufu watakiwa,
Na waliokwishajaliwa, si muhali nakwambia,
Hapa nilipofikia, kisomo nishawapatia,
Haramu haitozaa, halali kilichokua.

No comments: