Tuesday, November 15, 2011

Mungu atakalo huwa

Mola aliloamua, ndilo linalotokea,
Ila shetani hupewa, watu wa kuwachukua,
Uroho walojaa, na tadi kuwapofua,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Tamaa walojaa, shetani huwatumia,
Mamlaka kukwapua, kwa ya kwao manufaa,
Sheria kujitungia, za dhuluma na hatia,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Kamba hujakuachiwa, wenyewe kujinyongea,
Si manani kazubaa, itihari kawaachia,
Na nari haitochagua, kumeza wanaojizuzua,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Watakaoshindania, kuitawala dunia,
Matamanio kuzaa, pepo yanayoiondoa,
Muumba hatachelewa, watakayo kuachiwa,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Kiasi huwavumilia, hadi siku kuingia,
Wenyewe hujizodoa, huku wakilialia,
Milango ikifunguliwa, motoni wataingia,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Na nchi ilolaniwa, kwa ufisadi na hadaa,
Mola hujawaridhia, wabaya kuwachagua,
Maovu waliojaa, na mema wasonukia,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Muumba huwagawia, mnachokistahilia,
Vinginevyo mngepewa, wazuri walokuwa,
Sisi wenyewe raia, madhambi yametujaa,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Sisi wenyewe raia, madhambi yametujaa,
Hata viongozi pia, wa dini waliokuwa,
Wote wenye roho mbaya, bwana tusomsujudia,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Haya yanayotokea, wenyewe tumeandaa,
Budi kuyavumilia, huku toba tunaitoa,
Ili mola kutuvua, na hii ya wovu kofia,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Masharifu na watawa, muanze kujitambua,
Muache nanyi tumiwa, mnaiongeza balaa,
Ni nani ataongoa, ikiwa nyie mwavia?
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Nzuri yetu Tanzania, ila Mola hatujamjua,
Nia yetu kwake mbaya, na bado avumilia,
Ila mwisho utatua, wingule kuliepua,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Muumba kumrudia, bora kuliko kuchagua,
Mwaona mnavyopewa, uoza vilivyokua,
Na haya kuendelea, na nchi kudidimia,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

Neema tusipojua, mabaa tutayajua,
Mikosi na nuksi pia, tutafunga nazo ubia,
Haya yakawa ni njia, wenyewe tulochagua,
Mungu atakalo huwa, sio atakalo mtu!

No comments: