Kijana 'nachokosea, wengine kutegemea,
Wenyewe wanachojua,ya kwao kujifanyia,
Muda ukibakia,mke, watoto na jamaa,
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa!
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa.
Hilo halitatokea,unakubali hadaa,
Njia kuzifikiria,ni wapi utaanzia
Kijana 'nachokosea, kudhani wapo watenda!
Hawapo wakuelewa,njaa isiyowasumbua,
Ufisadi umejaa,matumbo bado yapwaya,
na vyama vimeingia,wizi na kutubagua,
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa!
Elimu kujipatia, lazima kusimamia,
Vituo kuvifungua, wenyewe kujiendeshea,
Wafadhili watatua, na msaada kugawiwa,
Kijana 'nachokosea, kudhani wapo watenda!
Mikopo wanaopewa, si nyie mnaotakiwa,
Vigogo waichukua, na vizito nao pia,
Ya kwao benki watia, chenu kidogo wakwaa,
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa!
Benki mkifungua, wazazi watachangia,
Mkiendesha murua, misaada mtaizoa,
Utumwani kukataa, wenyewe kuja ingia,
Kijana 'nachokosea, kudhani wapo watenda!
Siasa za chama mbaya,mbali kuzipatilizia,
Nyie wote Watanzania,iwe moja jumuiya,
Lengo lenu kuwa moya,kataeni kutumiwa,
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa!
Machinga mtawaokoa, na wengine kufatia,
Ujasiriamali kupaa, na nchi kuendelea,
Msikubali hadaa, serikali nayo yapewa,
Kijana 'nachokosea, kudhani wapo watenda!
Wapewa na wasinyaa, ukimwi utadhania,
Nyie kiu chawaua,kufuja mtakataa,
Kizazi mtakiokoa, na fedheha ya kuishiwa,
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa!
Mashirika wachagua, watoto wawaliopaa,
Nyie yatima mtakuwa,bila ya kujiangalia,
Ajira mkafikiria, wenyewe kujaziandaa,
Kijana 'nachokosea, kudhani wapo watenda!
Kijana Mtanzania, salama nakuamkua,
Amka ninakwambia, au waja angamia,
Amsha wenzako pia, ajenda kujijengea,
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa!
Ajenda kujijengea, na mtakavyojikomboa,
Bila ya kumtegemea, mjomba au majaliwa,
Nchi mtajaibiwa,huku bado mwasinzia,
Kijana 'nachokosea, kudhani wapo watenda!
Daima nawaswalia, yasije yakatokea,
Ninazisoma dua, maovu kujayaambaa,
Namuomba Jalia, taabu kuziondoa,
Kijana 'nachokosea, kudhani utafanyiwa!
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment