Ushairi huu dawa, wakubwa waikataa,
Kunywa yawachachafya,na matapishi kutoa,
Homa kali kuwatia, na wengine kupagawa,
Ushairi huu mpya, wababe hawaujui.
Utunzi usiosifia, wala kulamba wazawa,
Wababe kuwababua, na watu kuwazindua,
Unaoita kinyaa, kwa jina la kuzaliwa,
Ushairi huu mpya, wakubwa hawaujui.
Utunzi usovimbiwa, kwa hidaya za kupewa,
Mambo unaochambua, na mawe kuyanyanyua,
Na chini kwendafukua, ya chini juu yakawa,
Ushairi huu mpya, kuwadi hawaujui.
Utunzi usotulia, wahaha kila mtaa,
Majina kuyang'amua, watu wanaowahadaa,
Mijizi inayojitia, uchamungu kuvaa,
Ushairi huu mpya, dhalimu hawaujui.
Ushairi wa kufaa, shuleni kufafanua,
Vichwa kuvifungua, na kweli kujaijua,
Wanafunzi kukomaa, kwa hoja watakazozua,
Ushairi huu mpya, fisadi hawaujui.
Utunzi usosujudia, cheo wala majaliwa,
Haki uliochagua, urafiki nayo kuwa,
Vinginevyo tantabelua, vitu vya kuvua na kuvaa,
Ushairi huu mpya, majizi hawaujui.
Ushairi maridhawa, kuoza haitakuwa,
Kizazi hiki kufaa, na vijavyo manufaa,
Sanaa kupokelewa, hadi mwisho wa dunia,
Ushairi huu mpya, waongo hawaujui.
Twamsujudia Alaa, juu asiyefikiwa,
Na huko alikokaa, neema hutushushia,
Dunia kuangalia, wabaya akawajua,
Ushairi huu mpya, mkoloni haujui.
Mwisho huwaandikia,mzuri usiokua,
Na nari huwalilia, makazi kuwagawia,
Na hawa wasiojua, nini tutawasaidia?
Ushairi huu mpya, mkoloni haujui.
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment