Nauliza nisojua, wanasheria nchini,
Hivi ikijatokea, aliyemadarakani,
Katiba kuipindua, kwa vyake kuvibaini,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Kupanga na kupangua, vifungu vya ibarani,
Apendavyo akatia, na kuongeza thamani,
Na anavyovikataa, akavitoa mwangani,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
La mtu hakusikia, wala yao kuthamini,
Yake ndani akatia, hata yasiyo thamani,
Kisha akatuambia, sasa ni sheria yakini,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Kwa unyonge kuridhia, wananchi majinuni,
Maguvu yakatumiwa, sheria kuiamini,
Kooni kusukumiwa, kumeza tusihaini,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Macho tukifunguliwa, na uovu kubaini,
Hata zitachukuliwa, dhidi yao wahisani,
Adhabu kujapangiwa, sawa nao wahaini,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Kama ni chama twajua, haya kilichosaini,
Na wafuasi wakawa, bado wamo duniani,
Je, kujawachukulia hatua tutajawini?
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Mwenyekiti twamjua, aliyekuwepo nani,
Na wake mwanasheria, naye sio mtu mgeni,
Je, shtaka tutawasomea, kuwatupa gerezani,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Mangimeza walokua, wamekalia mezani,
Vipi kujawaokoa, wasiwe nao shtakani,
Au mkenge kwingia, kwa uovu kuauni?
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Nahisi yanatokea, haya ninayobaini,
Kimya kimya yawa, na nchi sasa hatarini,
Nani atakayefichua, yote yawekwe nuruni?
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Unguja wametangulai, hili sote twabaini,
Mengi wameamua, wanacnhi ngali gizani,
Na sasa wanatumia, bila kura ya maoni,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Tanganyika twashuhudia, mijini na vijijini,
Sheria wanavyofua, kuzipasi na kughani,
Kila nikifikiria, vyanukia uhaini,
Mapinduzi kikatiba, nao siyo uhaini?
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment