Monday, November 14, 2011

Vipofu wanageuka

Kuona vigumu hua, licha macho nayo kuwa,
Hongozi ikizidia, hakuna asiyelewa,
Chakari wote hulewa, wanofanya kutojua,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Mungu akishachukia, shetani atamwachia,
Na mtu akadhania, ya kwamba amejaliwa,
Kumbe moto apalia,kwa mawe yanayoungua,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Motoni wengi huingia, vyeo waliojaliwa,
Kwa kushinda zingatia, haki za chini walokuwa,
Wachache wanojua,mkumbo wanafuatia,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Hoja watazisikia, wala hawataelewa,
Milango hufunguliwa, na hushindwa kuingia,
Huoneshwa hata njia, wasijue pa kuanzia,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Shetani huwatangulia, kwa yote wakiazimia,
Huwafanyia mzaha, nyikani wakapotea,
Waamini wanajua, kumbe maaluni wawa,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Sodom na Gomorrah, haya yalikwishatokea,
Ya haki walikataa, haramu wakalilia,
Ndiyo yanayotokea, viso halali mwapewa,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Kitanzi wakitungua, na sasa wanakivaa,
Dahari wategemea, wataendelea kuwa,
Ila Muumba ajua, kwanini mchwa apaa,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Nani wa kumtegemea, kama hutotusikia,
Mola wetu unajua, moyoni yaliyojaa,
Bure kukusimulia, jamala twaingojea,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

Mkuu uliyekuwa, wa mbinguni na dunia,
Gumu halijatokea, ukashindwa kutatua,
Yasubiri Tanzania, hukumu kuiridhia,
Vipofu wanageuka, wazima walozaliwa.

No comments: