Tuesday, November 8, 2011

Anzisheni chama chenu

Vilivyopo vyazeeka, vyama vyetu Tanzania,
Baadhi vyahamanika, ushindani vyahofia,
Teknohama vyazika, hawana wa kutumia,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Imeshafika miaka, uongozi kuutwaa,
Demokrasia kushika, watu wakaviondoa,
Ila lataka hakika, kujua mnalojua,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Nchi badala yataka, ila haijatokea,
Bado mtu hajazuka, kazi anayeijua,
Na chama hakijafika, njia kinachotambua,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Vijana mwahitajika, jahazi kuliokoa,
Na hamsini miaka, muwe hamjaivuka.
Kizazi tunachotaka,cha uhuru kilichokuwa,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Nchi sasa inawataka, wazee kuwaondoa,
Watu wameshawachoka, na wala hawana jipya,
Kusinzia na kufoka, ndicho wanachokijua,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Jumuia tunataka, na chama nacho pia,
Nchi kitakachoiteka, vya zamani kuondoa,
Ili pawe na uhakika, kipo kizazi kipya,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Wasanii wasifika, chamani mwahitajiwa,
Washairi twawataka, na waandishi nao pia,
Walimu mnaoteseka, hapa ndio pa kuingia,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Madaktari twawataka, usukani kuushika,
Manesi wastahika, nyuma acheni bakia,
Wahandisi watajika, hataka mwahitajiwa,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Wanafunzi twawataka, sasa mnaodidimia,
Wafanyakazi haraka, chama kinawangojea,
Vijana mwahitajika, shamba mnaokimbia,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Kumekucha Afrika, vijana wanaingia,
Limepita lao rika, viongozi walokuwa,
Sasa zamu imefika, vijana kuwachagua,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Mikiki inasikika, wazee watakimbia,
Ukale umewashika, mapya wanahofia,
Sisi twataka kuruka, wao bado wanatembea,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Ujuzi tunaotaka, viwango hawajafikia,
Hata wazungu wachoka, chumi zinadidimia,
Vijana huko washika, nafasi zinazopwaya,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

Wazee waweweseka, matatizo yabakia,
Na kila wanapoamka, yawa ngumu Tanzania,
Vijana wahitajika, babu wapate pumua,
Anzisheni chama chenu, vijana wa Tanzania.

No comments: