Wednesday, November 23, 2011

Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Uongo tunajaribu, ufisadi tumeweza,
Wananchi kuwaghilibu, ili sisi kupendeza,
Wadhanie tu dhahabu, na wengine kapi chaza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Wakubwa wanahatibu, moyoni wasowekeza,
Linawamaliza gubu,na hasadi kuwaponza,
Muumba wamjaribu, naye hawatamuweza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Hata na akina babu, kwalo hili wanyamaza,
Uchama wawaadhibu, taifa walipoteza,
Na vichwa wenye harabu, jema wanalitangaza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Uongo waujaribu, malengo kuyapoteza,
Wa janibu na ghaibu, hakika wawashangaza,
Waonwa kitu cha ajabu, wengine kuwapakaza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Wameyakosa majibu, kwani si watu wa kuwaza,
Hawana haya na aibu,wananchi wawachuuza,
Na makubwa masahibu,katiba waigeuza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Katiba ina majibu, na hayamo kwenye giza,
Wananchi ndio habibu, mamlaka yatangaza,
Si rais na mahbubu,wapaswao kuyafanza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Si rais na mahbubu,wapaswao kuyafanza,
Ni wananchi taratibu, watakiwa kutangaza,
Kwa kuwatumia naibu,kazi watakaoagizwa,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Tume tukitaadabu, mkuu hatoifanza,
Atawaachia sulubu, wananchi kuitengeza,
Uchama usighilibu, kwa ajizi na mafunza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Twaisetiri aibu, haya si kwa Kiingereza,
Kajifunzeni adabu, au tutawapatiliza,
Watanzania kwa ghibu, sasa hamtawacheza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

Msifikiri mabubu, kwa magadi kuwasuuza,
Hakuna kwao ajabu, mkishindwa kuongoza,
Watafanya mjarabu, nchi ikajapendeza,
Tumeweza ufisadi, tunajaribu urongo.

No comments: