Thursday, November 10, 2011

Hekima za Makengeza

MZUNGU hutamjua, Kiswahili ni fasaha,
Kajaa Utanzania, CCM wazubaa,
Mwananchi aandikia, kejeli zisizochakaa,
Hekima za Makengeza, nani anazitumia?



Kwa hakika ninajua, walengwa hawajajua,
Na hata wanaojua, fikra hazijachanua,
Ni yaliyofunga maua, yangoja bado kuchanua,
Busara za Makengeza, nani achangamkia ?

Supupika amtumia, na wenzake waishiwa,
Hoja wanazozitoa, nchi zinaichambua,
Matatizo huibua, sugu yaliyokwishakua,
Hekima za Makengeza, nani anazitumia?

Fursa huzichambua, viongozi wazubaa,
Hakuna anayemtumia,ushauri kuwafaa,
Mambo yanaendelea, kawaida ilivyokua,
Busara za Makengeza, nani achangamkia ?

Husoma na kujicheka, kitu hawajaambulia,
Nchi yazidi makiwa, na makala zinajaa,
Hakuna linalotokea,ila wazidi sinzia,
Hekima za Makengeza, nani anazitumia?

Penye miti tunajua, wajenzi hupaambaa,
Ndivyo inavyoelekea, kejeli zinasinyaa,
Uchungu waliokuwa, ndio ndani wanatiwa,
Busara za Makengeza, nani achangamkia ?

Uoga watuzingua, uovu twavumilia,
Panya tumekwishakua, mapaka twawakimbia,
Nchi inateketea, hakuna wa kuitetea,
Hekima za Makengeza, nani anazitumia?

Makengeza endelea, vijana watasikia,
Na wakishakuelewa, hatua watazichukua,
Pengine watatuzindua, tufanze yanayofaa,
Busara za Makengeza, nani achangamkia ?

No comments: