Wednesday, November 30, 2011

Maji hakika uhai

Uhai maji hakika, pale yanapotulia,
Maji yakishatoweka, uhai unapotea,
Jambo hili si dhihaka, twafaa kuzingatia,
Maji hakika uhai, twapasa kulitambua!

Bakhressa si dhihaka, hili kaling'amua,
Jina alilopachika, sadifu linshakua,
Atamlipa Khalaka, na Muhyi alokua,
Maji hakika uhai, twapasa kulitambua!

Wengine wana wahaka, biashara watambua,
Wataka kutajirika, kwa mito nayo mvua,
Mungu anavyovitaka, bure bure vingekua,
Maji hakika uhai, twapasa kulitambua!

Serikali kujengeka, maji budi kuyatoa,
Vyanzo vikalindika, vya mito nayo mvua,
Pasiwe nayo mashaka, katika hii dunia,
Maji hakika uhai, twapasa kulitambua!

Haya yakitengeneka, uchumi tutaunyanyua,
Maji yatajauzika, kwa nayo wasiokua,
Nchi ikatajirika, mara fumba na kufumbua,
Maji hakika uhai, twapasa kulitambua!

Nadhani limeeleweka, fanya kinachotakiwa,
Acheni kujishobodoka, na ovyo kushangilia,
Nchi malezi yataka, sio wasanii kua,
Maji hakika uhai, twapasa kulitambua!

No comments: