Thursday, November 10, 2011

Robo bilioni gari

Hawa ni wetu watani, hivi ndivyo wajikita,
Ubaya hawauoni, shule kiwete yatweta,
Gari robo bilioni, ofisi analipata,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Uongozi sasa shani, watu wapenda kunata,
Ni bai umaskini, karibu kumetameta,
Ubinafsi unawini, utu wazidi zorota,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Kashfa hawajaita, kwao sifa na nishani,
Wananchi wanachokipata, shilingi kufa thamani,
Na bei zinatokota, fukra kikaangoni,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

KIpaumbele chadata, na hakiko fikirani,
Bendera upepo yafata, ya mweusi mkoloni,
Ni bure wanayoteta, twawajua kwa undani,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Wenyewe mkishaukata, watu hamuwathamini,
Ndugu zenu mwawavuta,wake, binti na zenu bani,
Wengine mwawaokota, wangoje hadi mwakani,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Kesho yenu kuikuta, hilo sio yumkini,
Mtazidi kupepeta, sisi ni makaburini,
Chuki inanisokota, mjamaa siamini,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Si nyie tuliwaita, wajamaa wajamani?
Vipi mnasakata, ubepari mwaamini,
Kulimbikiza mwateta, wala haya hamuoni,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Tumebki nyatanyata, tumekuwa hayawani,
Twawaogopa wakata,mmekua mumiani,
Damu mnaitafuta, ukwasi kuubaini,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Hata wabunge wang'ata, wamekwama mtegoni,
Kutuwakilisha wasita, waigiza redioni,
Televisheni waota, kuzidi kutuzaini,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Ninaicheza karata, kipofu kala na nani?
Na mkono kauvuta, nyama kutua sahanini,
Mwenzake akiokota, ngumi iko mdomoni,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

Viziwi wapiga kwata, nafuu hawaioni,
MbuzI kucheza gitaa, haijawa duniani,
Wavutao wakivuta, huna ila kwenda chini,
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

HIsia zitawakong'ota, joto lipande mwilini,
Maamuzi mnasita, kikaango ki jikoni,
Mitihani mkipita, nani atayaamini?
Robo bilioni gari, shule haina kompyuta!

No comments: