Dini hii ni tajiri, imekosa uongozi,
Yajifanya fakiri, yapamia udowezi,
Wafuasi kuadhiri, wakakosa utambuzi,
Dini hii ni tajiri, viongozi imekosa!
Udhibiti haujiri, hapanao wakaguzi,
Mahesabu ni kamari, kuyasoma huwezi,
Kila mtu jemadari, na mkuu kiongozi,
Dini hii ni tajiri, najisi wanasiasa!
Wasomi kwao kafiri, kushauri si ruksa,
Utaalamu si heri, mambo yenda kisiasa,
Ni ndefu sana safari, na sudusi hawajagusa,
Dini hii ni tajiri, nahodha inamkosa!
Wahasibu kwao shari, na kanuni si azizi,
Ni mrama manowari, langoja zama jahazi,
Kila nikitafakari, naliona jinamizi,
Dini hii ni tajiri, nahodha inamkosa!
Mikakati kwao shari, mipango na maamuzi,
Kila mtu jemadari, na mkuu kiongozi,
Dira kwao minghairi, kwenda mbele hawawezi,
Dini hii ni tajiri, arijojo imetoswa!
Demokrasia kijiri, katika zake chaguzi,
Kuwakwaza washihiri, na wengine wavamizi,
Huenda ikadhihiri, kujazuka kiongozi,
Dini hii ni tajiri, viongozi mamluki!
Ushindani ukijiri, madhehebu kuhafidhi,
Taasisi kuabiri, kujafanya zao kazi,
Waumini minghairi, watayatoa machozi,
Dini hii ni tajiri, viongozi ni mbumbumbu!
Mapinduzi ya dhahiri, budi uwe uamuzi,
Yafanyike yenye kheri, dini ije anza kazi,
Anga zote kuabiri, tukatae udowezi,
Dini hii ni tajiri, viongozi imekosa.
Elimu tuikariri, kujifunza uongozi,
Na hii kubwa bahari, kuogelea ni kazi,
Ila yapo taksiri, ya mbinu na ujuzi,
Dini hii ni tajiri, viongozi imekosa.
Haitoshi kukariri, elimu ya mazoezi,
Lazima pia kujiri, mabingwa na wajuzi,
Mambo yetu kimahiri, wajaribu kuyaenzi,
Dini hii ni tajiri, viongozi imekosa.
Ushehe na udaktari, tusifanyie ajizi,
Hizi pacha mashuhuri, kwa mjinga haangazi,
Haya yakitasawari, dini itapanda ngazi,
Dini hii ni tajiri, viongozi imekosa.
Uchamungu kidhihiri, yataondoka masizi,
Imani kuwa na heri, na baraka za Mwenyezi,
Zitaondoka na shari, ichekelee ardhi,
Dini hii ni tajiri, viongozi imekosa.
Usafi wa maamiri, ni kwa wao uokozi,
Iweje uwe kafiri, wahihaki wenye enzi,
Au mkuu hasiri, wamdhihaki Azizi,
Dini hii ni tajiri, viongozi imekosa.
Uadilifu dahari, kuwa wetu uongozi,
Kiasi tusikithiri, haya makubwa majazi,
Alitambua Qahari, alo mwingi wa ujuzi,
Dini hii ni tajiri, ila hamna viongozi!
Maskini kwa tajiri, wazee tuwaenzi,
Na shura waiajiri, zaka na mali kuhifadhi,
Pasiwe nayo ghururi, nyoyo ziwe mahfudhi,
Dini hii ni tajiri, viongozi waiuza!
Baitul mal ijiri, hazina kuienzi,
Iundiwe na urari, salio kulimaizi,
Kwani bila daftari, mali watatwaa wezi,
Dini hii ni tajiri, viongozi wahujumu!
Sadaka iwe hiari, tusifanye ulanguzi,
Twajitia ujibari, kufosi hata wakazi,
Hapendi haya Akhiri, haya kayaweka wazi,
Dini hii ni tajiri, viongozi walakini!
Zaka hii ni amri, waumini waienzi,
Kila pato likijiri, ifanyie maamuzi,
Baitul mal pazuri, wacha Mungu wakabidhi,
Dini hii ni tajiri, viongozi ndio kupe!
Mali ikidhihiri, tuwekeze kikombozi,
Shule kuzitafakari, zenye viwango azizi,
Na vyuo kuvidahiri, vilivyo na kubwa hadhi,
Dini hii ni tajiri, viongozi ombaomba!
Maji kwetu ni johari, tuyatafute Chamanzi,
Mifereji kuajiri, na bomba kwenye makazi,
Kuongeza utajiri, waumini iwe kheri,
Dini hii ni tajiri, viongozi wanakiri!
Umeme tuutabiri, kuuzalisha si kazi,
Hata tukiajiri, wazungu wenye ujuzi,
Shughuli izae heri, giza likose makazi,
Dini hii ni tajiri, viongozi taabani!
Hosteli tukasiri, wenetu kuwahifadhi,
Na misikiti kujiri, kwenye salama hifadhi,
Kuswali wasisubiri, kwenda nje ya makazi,
Dini hii ni tajiri, viongozi masikini!
Biashara tuabiri, ajemi hadi Uholanzi,
Na wengi kuwashauri, kuanza nayo makuzi,
Ili nasi tusafiri, alikopita kipenzi,
Dini hii ni tajiri, viongozi ni dhaifu!
Tuesday, November 8, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment