Friday, November 18, 2011

Ibilisi ashangaa

Profesa wa hadaa, ibilisi ashangaa,
Twamshinda Watanzania, kwa umbeya na hadaa,
Uzaini tunaulewa, malengo yetu yakawa,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Siasa zetu balaa, uongo tunavyotumia,
Viongozi wanajua,na bado waendelea,
Ni wagumu kutubia, watanguliza dunia,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Nini watatuambia, wakubwa waliokua,
Eti wabambikiwa, ukweli hawakujua,
Au ni wakubwa wabia, kwenye dhambi ya hadaa?
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Watu tumekomalia, nafsi kuzipaua,
Na aushi ya hadaa, miaka isochukua,
Ovyo yanayodidimia, tetemeko 'kitekea,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Ukweli tunaujua, lakini twaukataa,
Maamuzi kuamua, Khafidi akachukia,
Hasara yetu ikawa, hadi mwisho wa dunia,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Uongo twautambua, bado twaukubalia,
Dhuluma ikaenea, kila kona kusambaa,
Wanyonge kumlilia Alaa ada ikawa,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Ibilisi asomea, kwayo tuliyobobea,
Mengine hakuyajua, hadi macho kumfumbua,
Elimu ajipatia, viumbe tuliojaliwa,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea

Elimu ajipatia, viumbe tuliojaliwa,
Ibilisi amekuwa, mwanafunzi mwaminiwa,
Kutamba kunapungua, viumbe wamtangulia,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Kila anapoingia, sisi tunshapitia,
Na mwengine yamwia, vigumu sana kujua,
Abakia ashangaa, cheo tulichojipatia,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Ushamba tumemtoa, wamjini twaingia,
Na pindi tukiziwa, nguvu tutatumia,
Naye kumgeukia, kuja kutusaidia,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

Mwanadamu ninalia, k.o. kujipatia,
Ibilisi kumtoa, raundi mwanzo ilokuwa,
Na sasa twaendelea, taji kubwa kujapewa,
Ibilisi ashangaa, uongo tulivyobobea.

No comments: