Friday, November 18, 2011

Zawadi ya udhalimu

Hili si utaalamu, wala hadithi yabisi,
Aelewa mwanadamu, hedaya yake maasi,
Mkuu wa mahakimu, kaukana ni najisi,
Zawadi ya udhalimu, ni nuksi na mikosi!

Akiwa mwongo imamu, maamuma muflisi,
Na wanaotakadamu, huishi kwa wasiwasi,
Haitulii kaumu, madhali kuna nakisi,
Zawadi ya uzaini, ni nuksi na mikosi!

Kadiri kitu muhimu, nayo yataka kiasi,
Wanatwambia walimu, kitu hiki ni balansi,
Mahala isipodumu, sio njema majilisi,
Zawadi ya udhalimu, ni nuksi na mikosi!

Si taabu kwa Alimu, aliye bora Qudusi,
Jambo hili kaukumu, alipoasi Ibilisi,
Na hadi leo ladumu, kwa ngumbaru na mamajusi,
Zawadi ya uzaini, ni nuksi na mikosi!

Wala halinayo zamu, wala nusu na sudusi,
Hili jambo la kiamu, wengi huwa lawaghasi,
Na wakubwa madhalimu, huwatoa makamasi,
Zawadi ya udhalimu, ni nuksi na mikosi!

Walopewa uadhimu, wakaiivua lebasi,
Wakalifanya haramu, halali kiujasusi,
Viumbe kuwadhulumu, na maovu kuasisi,
Zawadi ya uzaini, ni nuksi na mikosi!

Hukasirika Rahimu, akaishusha nuksi,
Dhiki isiwe admu, kwa balaa na mikosi,
Na nchi ikesha hamu, na kujaa kinamasi,
Zawadi ya udhalimu, ni nuksi na mikosi!

Waulize wakarimu, mambo wanaodadisi,
Walo huru na hadimu, aya wanazo fususi,
Wala haikugharimu, bure waweza durusi,
Zawadi ya uzaini, ni nuksi na mikosi!

No comments: