Thursday, November 10, 2011

Serikali ya kihuni

Naapa hayumkini, wapo wafanya uiani,
Vya maana hawabuni, sasa ngumi mikononi,
Kazi kutiana ndani, askari wakawini,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Sheria za kikoloni , zatuweka mashakani,
Nchi iko taabani, muokoaji ni nani,
Kazi hawaithamini, siasa sasa ni dini,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Hutumia milioni, kufanyiana uhuni,
Kukomoana mjini, tujue bosi ni nani,
Tupatacho maskini, shilingi kushuka thamani,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Huduma zetu ni duni, usalama hatuoni,
Wetu sasa wakoloni, vituko wanabaini,
Imetoweka hisani, uchumi u kitanzini,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Ahadi zimesakini, kifanywacho hatuoni,
Watu hawaandamani, kisa hatujakibaini,
Mikutano hatiani, haki hatuithamini,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Twashindwa na baniani, kiatu chake auni,
Ajira hatuioni, na mikopo kizimbani,
Matunda yote mtini, wala walo kileleni,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Benki kuu hazinani, fedha haionekani,
Ukija na mitaani, mifuko ni matoboni,
Bei zapaa angani, ununue kitu gani?
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Pikipiki mitaani, ni kadhaa majiani,
Wanaendesha kihuni, sheria haijulikani,
Bajazi nazo njiani, usalama mashakani,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Daladala za kihuni, wamiliki ni wahuni,
Wengine eti yakini,mabosi serikalini,
Utawafanya nini, na nchi yao jamani?
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

Tunusuru ya Manani, dira imerizaini,
Hatujui njia gani, tunapelekwa duniani,
Jahanamu naamini, na wala sio peponi,
Serikali ya kihuni, itazalisha uhuni!

No comments: