Wednesday, November 9, 2011

Mwanangu kuhusu kazi

Babayo mfanyakazi, huwezi chagua kazi,
Pale unapobarizi,ifanye ni yako kazi,
Pata tonge na mchuzi,mengine omba mwenyezi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Zimepita zake enzi, mtu kuchagua kazi,
Hata walio wajuzi, ni kazi hawaliwezi,
Ipatikanyo kazi, ndiyo hiyo ya kuienzi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Ni wale wenye wazazi, wenye viwanda na majenzi,
Ndio tu sikuhizi, wawezao ubaguzi,
Vinginevyo ni kizazi, kwa lolote baingizi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Au wana wa viongozi, kujawarithi wazazi,
Hawahitaji ujuzi, ila jina la baba mzazi,
Huhitaji king'amuzi, hili nalo kumaizi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Vizito wana majenzi, huyafanya mateuzi,
Vigogo nao si kazi, mtoto kumpa hifadhi,
Ila kama hawajiwezi, yabaki masimulizi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Darizi sana darizi, yaweza kuwa kazi,
Vua hata na mkizi, uvuvi kuwa majazi,
Chunga ng'ombe na mbuzi, ufugaji uwe na hadhi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Ila usiwe ni mwizi, au siasa jambazi,
Yafate yako malezi, mola kuwa ni mwokozi,
Halibaki tupu zizi, hata penye uvamizi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Kibirizi, kibirizi, usiamini hirizi,
Ushirikina upuuzi, hautakupatia kazi,
Akili ipe zoezi, mganga hajajienzi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

Yashone nayo mavazi, na mitumba udarizi,
Ukipata wanunuzi, tayari unayo kazi,
Maji ukiwa mchuuzi, riziki haina kazi,
Mwanangu kuhusu kazi, huchagui sikuhizi!

No comments: