Sunday, November 27, 2011

Mbunge mrembo?

Akili tumeamua, zitue kwenye jukwaa,
Kupambana kwa hatua, na sura inavyokua,
Tuone wa kunyakua, ushindi nani atakua,
Ni nani mbunge mrembo, shindano kimataifa ?

Kama vile mabondia, nao watashindania,
Akili awe kulia, na kushoto sura kua,
Wapambane kishujaa, hadi atakayezidiwa,
Ni nani mbunge mrembo, shindano kimataifa ?

Hadi atakayezidiwa, ubingwa kuutwaa,
Ngao akaichukua, ukutani ikakaa,
Wanawe wakatambua, bingwa alikwishang'aa,
Ni nani mbunge mrembo, shindano kimataifa ?

Ndani tuajaingia, nini kazungumzia,
Kilicho cha manufaa, kwa wenzake Watanzania,
Na siku alipotoa, mada isiyosinyaa,
Ni nani mbunge mrembo, shindano kimataifa ?

Vigelegele ikiwa, maksi hatozipewa,
Sifuri kuambulia, na zomeo la jukwaa,
Macho chini akatua, atakavyoumbuliwa,
Ni nani mbunge mrembo, shindano kimataifa ?

Na kama ilitokea, mwenyewe kujitanua,
Ubinafsi kulea, na umimi kubobea,
Jukwaa litamzuzua, kwa miluzi na nazaa,
Ni nani mbunge mrembo, shindano kimataifa ?

No comments: