Nafsi yako chunguza, ukweli utaujua,
Huna uliloliweza, wenda nyuma kwa hatua,
Pabaya watubamiza, hatuna pa kupumua,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Shilingi umemaliza, thamani imepungua,
Bei unazipaaza, hakuna wa kukutia,
Kupona ni muujiza, kufa tunakungojea,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Gharama umezikuza, hali zinadidimia,
Hatuna tunaloweza, bila watu kutegemea,
Nchini twaona giza, nuru yazidi potea,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Uongozi umeviza, chama na Tanzania,
Kila kitu ni kukwaza, hakuna linaloelekea,
Mgongo tumegeuza, mafuta kupakaliwa,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Itakuwa muujiza, dhahabu bure kutoa,
Kisha nchi kuikuza, na nafuu kuingia,
Hadithi hii ajuza, naye atakubishia,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Vipi yanakushangaza, kilio tunacholia,
Kama uchumi wakuza, hali sizingetengemeaa,
Twaona tunaburuzwa, afueni twasikia,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Wapambe kuwapuuza, ukweli utaujua,
Kijijini ukitokeza, dhuluma utaivaa,
Unyonge unatukwaza, nawe hili hujajua,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Acha ya watu kumeza, macho yako kufungua,
Njoo uje kusikiza, siyo hayo ya kuambiwa,
Ghafla shitukiza, kama nawe hujalia,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Shilingi yatutatiza, vipi mia kuijua?
Misaada mnayotunza, wala unaowajua,
Kwetu haijapenyeza, wala haijatufikia,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Ya Hatuna fatiliza, mwana Rashid maridhia,
Mjini kujitembeza, matambara umevaa,
Kijijini kutosaza, kwenye sura ya bandia,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Hamsini twakeleza, sisi hatutafurahia,
Fanyeni mnayoweza, hatuna la kushangilia,
Ni bure tutajawakaza, nyie nchi mlotwaa,
Chunguza nafsi yako, ukweli utaujua.
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment