Wednesday, November 30, 2011

Uchafu tumezoea

Usafi huwa tabia, mbali inayotokea,
Ukijenga mazoea, akilini hubakia,
Huna utaloamua, bila ya kuzingatia,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Uchafu usipotia, pahala hapana doa,
Ila hapo ukiachia, pachafu patajakua,
Usafi njema tabia, uchafu unazuia,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Binafsi watakiwa, usafi kuangalia,
Nia kutokulegea, hata ukiwa mkiwa,
Na ukajihudumia, ukawa ni mashalaa,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Si nje unaanzia, bali ndani unakokaa,
Vitu vyote vyatakiwa, daima safi vikawa,
Kuvipanga ni murua, si ovyo vikasambaa,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Muhimu pakafagiwa, na bora ni kudekiwa,
Taka ukajizolea, mbali ziende tupiwa,
Nyumba yote ikang'aa, na vizuri kunukia,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Nje nako kufagia, taka kutokuhamia,
Na kisha panda maua, watu yanayovutia,
Kwa rangi zilizojaa, na harufu kunukia,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Bustani inafaa, kwa nyumba pia mitaa,
Na misitu manispaa, miti bora kupandia,
Hali ya hewa ikawa, ni yenye kutamaniwa,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Taadibu kwa wasia, na maneno ya kufaa,
Kwa uple simamia, na nyenzo kuwapatia,
Watu katika mitaa, uchafu kwao si nia,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

Ila ukivumilia, uchafu huwa tabia,
Watu wakaizoea, wasiwe nayo kinaya,
Yote waone ni sawa, pepo ikawa kinyaa,
Uchafu ni mazoea, huponywa na taadibu!

No comments: