Monday, November 14, 2011

Hongereni wawakilishi

Ukweli tumeujua, ni wapi wanalalia,
Na mengi tumegundua, hata na zao hadaa,
Yakini tunatumiwa, wakubwa kuwajengea,
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

Kasri wajijengea, au kuja zinunua,
Kaburini kujengea, watakapotufukia,
Na minara yao kukua, dunia ikawajua,
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

Upande waliokua, madhali tunatambua,
Sasa twawasifia, vyeo wanshachukua,
Hongera kuwatupia, jinsi walivyonunuliwa,
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

Hongera twawatumia, wawakilishi nazaa,
Chama mwakisaidia, kiweze kutubagua,
Kutufanya ni majuha,hatuna tunalolijua,
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

Hongera wa kutununua, na kisha kujinunua,
Ila moto mkipewa, msije kutugaia,
Wenyewe kufurahia, nari mtakayojaliwa,
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

Macho wanaotufungua, wadaiwa kutuhadaa,
Nyie upofu mwatutia, ni vipi kuwatambua?
Ni Mola anayejua, naye atawazawadia,
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

Kusoma mnazidiwa, hoja zote zimepaa,
Kazi kushangilia, na vigelegele kubwia,
Wenyewe mmejichagua, nani amewachagua?
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

Nguo zetu mmevaa, ila wafu twawajua,
Ni wasiomsaidia, yule anayeteketa,
Ila humshindilia, akazidi angamia,
Hongereni wawakilishi, wa chama na serikali.

No comments: