Sunday, November 27, 2011

Nesi bora ?

Nesi analaumiwa, eti ana roho mbaya,
Na anaowaangalia, hali hawajamjua,
Mimi nachanganyikiwa, wapi pa kusimamia,
Nesi bora duniani, ni nani kimataifa?

Kazi yao ya dunia, hawana pa kutulia,
NI wapi watajakaa, wajaliwe kupumua,
Watu wanaugulia, huduma watarajia?
Nesi bora duniani, ni nani kimataifa?

Wengine wajichafua, kuogeshwa hutakiwa,
Wa kule wanangojea, na wao dawa kupewa,
Hawa wanasubiria, shindano kuja patiwa,
Nesi bora duniani, ni nani kimataifa?

Shida zimezidia, wengine wawa vichaa,
Au kubwa malaria, mtu inamsumbua,
Hapo kazi kubwa hua, kitandani kumvaa,
Nesi bora duniani, ni nani kimataifa?

Wengine kula balaa, lazima kusimamiwa,
Au mirija kutiwa, na kisha kumiminiwa,
Daftari zangojea, taarifa kuchukua,
Nesi bora duniani, ni nani kimataifa?

Operesheni huvia, nesi kama hatatokea,
Bosi huchanganyikiwa, asijue pakuanzia,
Nesi akishatokea, ni rahisi kazi huwa.
Nesi bora duniani, ni nani kimataifa?

Vijisenti twavitaa, yeye tupu abakia,
Mshahara wake njaa, na nyumbani ni balaa,
Hili hatujazingatia, lawama hizi mafua,
Nesi bora duniani, ni nani kimataifa?

No comments: