Wednesday, November 30, 2011

Wanawake Tanzania

Waoga walikimbia, au walondolewa,
Vyeo kutunukiwa, majuu wakaishia,
Ukubwa ulipokoa, watoto kazi kulea,
Wanawake Tanzania, iundeni Jumuiya.

Wengine wanatumiwa, na wakubwa walokua,
Zawadi wakigaiwa, mapambano yapotea,
Nchi inaangamia, nyie mnazainiwa?
Wanawake Tanzania, iundeni Jumuiya.

Uchama mnatakiwa, kabisa kuukataa,
Jumuiya kuizua, wanawake kuingia,
Bila mmoya kubagua, chama anachotokea,
Wanawake Tanzania, iundeni Jumuiya.

Maslahi ya radhia, hakika yafanania,
Vinginevyo haijawa, ila wanaopendelewa,
Wao watajivunia, kwa hivyo wanavyopewa,
Wanawake Tanzania, iundeni Jumuiya.

Wamoja mkishakua, nguvu mtajionea,
Milima mtabomoa, na madaraja kutua,
Nchi juu ikapaa, na jamii kupumua,
Wanawake Tanzania, iundeni Jumuiya.

Hamfai kubakia, sarawili kuivua,
Baba kumtegemea, na nyie mnshakua,
Waume mwatarajiwa, sasa kuja watumikia,
Wanawake Tanzania, iundeni Jumuiya.

Waume wanaowafaa, hawa wote Watanzania,
Sauti mkaitoa, hoja mkajijengea,
Na sio kushangilia, au wengine kuzomea,
Wanawake Tanzania, iundeni Jumuiya.

No comments: