Thursday, November 10, 2011

Mgonjwa hukumjali

Mgonjwa hukumjali, unajali kwenda zika,
Ni saa kumi na mbili, kilioni unafika,
Hukumjulia hali, kumsindikiza wataka?
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

Yaonekana ni hili, ulilokuwa wataka,
Ndotoyo sasa kamili, unawahi kwenda zika,
Kaburi halina mwali,kila mja lamtaka,
Hakika mwenye bahati, milele habahatiki!
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

Mtazame mswahili, tabiaye ni mikiki,
Kimbelembele kikweli, hata pawe hahusiki,
Ila sio hospitali, mauti hyadiriki,
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

Mgonjwa humwacha hali huduma astahiki,
Ila kwenda kula wali, siku ya mazishi haki,
Mila hii si akili, na wala sijaiafiki,
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

Ukweli naukabili, siogopi unafiki,
Ninaliona dhalili, tena lenye ushiriki,
Asiyekuwa na mali, ndio kabisa hawafiki,
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

Majilisi kulihali, udhalimu zashiriki,
Hawataki jua hali, kwenye kifo wanafiki,
Tiketi au kibali, ni mazishi kuhakiki,
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

Usiponijua hali, usinizike sitaki,
Ni haramu si halali, siutaki unafiki,
Kilio chako si kweli, ni uchuro haumezeki,
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

Asiyenijua hali, kwangu amekwishafariki,
Marhum ilhali, kwa yakini huniziki,
Baki na wako ahali, mazishi yangu hufiki,
Hukumjali mgonjwa, unajali kwenda zika?

No comments: