Monday, November 14, 2011

Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Siasa zimefubaa, viranja vipofu kua,
Hawajali Tanzania, ya kwao wafikiria,
Sasa waanza tugawa, kabla hatujajigawa,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Hadaa nchi yavaa, vazi linalowapwaya,
Na wakubwa kwa tamaa, ukweli waushangaa,
Juu chini imekua, nchi haitoendelea,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Nchi tunaipindua, ukubwa twauchukua,
Rais sio raia, katiba kusimamia,
Ni ubabe watumiwa, na uzaini kuzaa,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Raia wa Tanzania, wenzao wangechagua,
Toka chini kutokea, uwakilishi kupewa,
Makundi kila jamaa, kujawawakilishia,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Mdau mmoja katwaa, kwa mabavu kutumia,
Haki ya kujiandikia, mswaada usiofaa,
Kisha kung'ang'ania, wabungewe kutumia,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Hili naona kinyaa, na sintolikubalia,
Kizazi nakiambia, katiba ijayo baa,
Na mkiikubalia, taifa litapotea,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Wachache waliokuwa, vipi sawa na wengi kua,
Laki tisa twaambiwa, Zanzibar walokua,
Kisha ukubwa wapewa, ya kwetu kuja amua?
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Zanzibar ni mkoa, kwa kimo na yake hatua,
Vinginevyo haujawa, ni pulizo lililojaa,
Msikubali mikoa, kuburuzwa na kisiwa,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Mikubwa yetu mikoa, Zanzibar yazidia,
Nayo ingelifaa, uwakilishi swa kua,
Dhuluma twaikataa, na Mola aitambua,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Waumini twashangaa, kuritadi wamekua,
Hili washangilia, kama wanaotumiwa,
Kidogo walichopewa, kikubwa kimeshakua,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

Kizazi mwakisusia, wenyewe mwajiangalia,
Laana mnaichukua, na vizazi kufatia,
Wote mnaotuhadaa, ilhali mnajua,
Muswada unatugawa, itakuwaje katiba ?

No comments: