Wednesday, November 30, 2011

Chozi la mamba

NInaiona hadaa, viongozi wakilia,
Mjini watu wajaa, vijiji wanakataa,
Hali sote tunajua, serikali yachangia,
Watu mjini kujaa, chozi la mamba mwalia.

Viongozi wa hadaa, haya wanajitakia,
Siasa zinatuua, wao wanafurahia,
Uchumi wamekalia, kama mibweha walia,
Watu mjini kujaa, chozi la mamba mwalia.

Kila kitu wanagawa, mjini wanaopewa,
Vijiji vyaambulia, ahadi nazo hadaa,
Maporini kumekua, vigumu kuendelea,
Watu mjini kujaa, chozi la mamba mwalia.

Haya tiulipoanzia, Uyahudi nao pia,
HIvi leo wamekua, na vijiji maridhia,
Tofauti hutojua, kijijini ukikaa,
Watu mjini kujaa, chozi la mamba mwalia.

Kwetu nyikani twajua, tena ni gizani pia,
Umeme haujaingia, na maji ni tope hua,
Katika kuendelea, mimi hili nakataa,
Watu mjini kujaa, chozi la mamba mwalia.

Busara tungetumia, vijana wasingekimbia,
Mahitaji yangekuwa, shamba yameshaenea,
Huna la kukusumbua, kila kitu wanunua,
Watu mjini kujaa, chozi la mamba mwalia.

Nani angeliamua, kijijini kutokaa,
Mjini tungekimbia, arkadi kuvamia,
Hewa tuipate poa, kutengemaa zetu afya,
Watu mjini kujaa, chozi la mamba mwalia.

No comments: