Wednesday, November 30, 2011

Napuyanga Mmachinga

Mmachinga natembea, daima chini ya jua,
Kichwa kinaungua, sina pa kukimbilia,
Riziki nimenuia, ni lazima kuingia,
Napuyanga mmachinga, changudoa atanua!

Halali nimeamua, haramu sintochukua,
Serikali yaamua, mjini kuniondoa,
Bongo hawajatumia, mimi hilo ninajua,
Napuyanga mmachinga, changudoa atanua!

Twaweza kusaidiwa, kivutio tuje kuwa,
Watalii kutujia, na vitu kuvinunua,
Nchi juu itakuwa, na uchumi utapaa,
Napuyanga mmachinga, changudoa atanua!

Akili wameamua, likizo kwenda kukaa,
Vitu kufikiria, uvivu wameshaingia,
Maamuzi kuamua, masikini waje lia,
Napuyanga mmachinga, changudoa atanua!

Napuyanga, natembea, nimezibeba bidhaa,
Watu nawafikishia, hadi wanakotokea,
Nyumbani kuwafikia, nafuu kuwapatia,
Napuyanga mmachinga, changudoa atanua!

Mimi sijaheshimiwa, ila wao changudoa,
Magari wawanunulia, na mitaani kung'aa,
Uchumi sijaelewa, nini wanachochangia,
Napuyanga mmachinga, changudoa atanua!

Atanua changudo, Mmachinga natembea,
Nani kunisaidia, hali akaninyanyua,
Mwanamke sijakua, labda wangetokea,
Napuyanga mmachinga, changudoa atanua!

No comments: