Monday, November 14, 2011

Binzari

Mbona ya kwako manjano, hali yangu ni nyekundu,
Hapanao uwiano, au huu ni utundu?
Ni tofauti unono, au vyote ni chachandu?
Binzari yangu njano, mbona ya kwako nyekundu?

Au ni wangu uono, na na rangi hii utandu,
Ikiwa hauna meno, vipi utafune nundu,
Hujui piga piano, vipi usiwe kingwendu?
Binzari yangu njano, mbona ya kwako nyekundu?

Mia sio miatano, chururu ni bandubandu,
Uvimilivu kivuno, waridhikao matandu,
Nayo mafuta ya mbono, hayajawa ya ukindu,
Binzari yangu njano, mbona ya kwako nyekundu?

Mwulize Haji Machano, aliyeishaumwa na tandu,
Sijui hili agano, la manjano na wekundu,
Naona ni utengano, wewe na jambia mimi mundu,
Binzari yangu njano, mbona ya kwako nyekundu?

Siwezi sema si neno, ananielewa Pandu,
Keshaniunga mkono, anaitumia Jandu,
Waogopa kisonono, ukimwi wafanza utundu?
Binzari yangu njano, mbona ya kwako nyekundu?

No comments: