Tumbo lakuchahia, kwa haya kuyasikia,
Mwenzangu nakuhurumia, dawa nitakupatia,
Ila uzidi sikia, yale usiyoyajua,
Tumia bakalhadi, pengine utajapona.
Mujarabu na radhia, hii mahsusi dawa,
Kanuni ukiijua, na vyema kuitumia,
Maumivu hupotea, salama ukabakia,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Maji ukiyatumia, safi sana yatakiwa,
Na wanaokusaidia, wachafu kutokuwa,
Umaridadi ni riha, kitu hautosaidia,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Unga ukishasagia, maji utachanyia,
Kijiko kukorogea, hadi rangi ikakoa,
Nyeupe isiyo waa, na kisha chini kutulia,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Vijiko viwili tumia, kabla ya kusinzia,
Na usipojisomea, vitatu vitakufaa,
Na kama mteuliwa, vinne wawajibiwa,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Uongo ukinuia, dawa haitakufaa,
Ubishi wa kutumiwa, dawa itakuumbua,
Vigelegele kitoa, utaumwa na kifua,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Chama ukishangilia, utazidi kuugua,
Sahau walokuchagua, dawa sumu huja kuwa,
Ubinafsi kurubia, kaburi hukuchimbia,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment