Wapi siri huanzia, na wapi inapoishia,
Watumishi mlokuwa, vipi bosi mwamhadaa,
Vipi mtaniambia, yangu hamtaniambia?
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Kazi nimewapatia, sasa mwanisasambua,
Eti mnashuhudia, pembeni mmenizoa,
Hamtaki nikajua, lile mnaloliamua,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Hivi mimi Mtanzania, na nchi nasimamia,
Vipi niliowateua, siri mnaniwekea,
Vipi nitawaangalia, muache kuniibia,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Iweje mkitumia, siri mnaniambia,
Nitajuaje raia, vyangu hamjasanzua,
Ubadhirifu ukiwa, vigumu kuuvumbua,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Mwauza mnavyojua, bei hamjaniambia,
Pasenti mwazichukua, na malipo mwayazoa,
Vipi mnaniambia, eti siri imekua,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Safari mwajigawia, zingine nisojua,
Mwaenda kwa mamia, milioni kutumia,
Kisha mnatangazia, ni siri hamtatoa?
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Za EPA mwaziepua, nayo siri imekua,
Huyo anayeniibia, mbona sijamnjua,
Ni chama au Mtanzania, aliyekwishalaniwa?
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Wengine nimesikia, bilioni mbili khaa!!!
Shuleni wamezitoa, watatu kwenda somea,
Ninashindwa kuelewa, shahada walochukua,
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
NI ya kufa na kufufua, shahada waliyopewa,
Vinavyokufa kufufua, hai tena vijekuwa?
Au yazidi sanaa,na mwizi kuachiwa?
Siri huanzia wapi, na wapi inapoishia?
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment