Wednesday, November 30, 2011

Mkopo kapewa nani

Mwenye dhiki sijapewa, mkopo kapewa nani,
Redioni nasikia, wametwaa bilioni ,
Denda nikalitoa, na kujaa tumaini,
Mkopo kapewa nani, mwenye dhiki sijapewa?

Majina kuyasikia, zikanichafuka mboni,
NI wakubwa walokua, na nyumba za uani,
Fukara sijasikia, nikadhani ni utani,
Mkopo kapewa nani, mwenye dhiki sijapewa?

Anyang'anywa asokua, alopewa hazinani,
Miguu juu ikawa, kichwa kikaenda chini,
Haya yanaendelea, dawa sijaibaini,
Mkopo kapewa nani, mwenye dhiki sijapewa?

Wadai wanaojua, hakopeshwi masikini,
Tajiri akichukua, mnakua si shakani,
Maskini akipewa, kurudisha yumkini,
Mkopo kapewa nani, mwenye dhiki sijapewa?

No comments: