Thursday, November 10, 2011

Serikali ya kibabe

HUJUI leo wajua, kusahau si uzembe,
Ya moyoni yako nia, sifazo ndizo ipambe,
Na waliokwishapotea, huuthamini ubabe,
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

Ni asili yake mja, kwa insana wampambe,
Na kula anayejua, hakamiliki kiumbe,
Pale anapokosea, ni umungu ajirembe,
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

Kwa yakini hudhania, hili hujakata ngebe,
Lakini hushtukia, debe tupu likilia,
Na sauti huibua, izidi hata mikebe,
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

Hili ukishalijua, utaogopa dungayembe,
Nalo ukifikiria, utaupata ujumbe,
Ukazijua ishara, bila kulevywa na pombe.
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

Maisha yetu kakara, budi mguu uvimbe,
Na katika kusakura, weza umizwa na wembe,
Na ikiwa ni majura, waweza katwa na jembe,
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

Yapasa Watanzania, Mola sana tumuombe,
Kuiondoa kadhia, ya vitimbi na vijembe,
Uungwana watu kuwa, ovyo ovyo tusitambe,
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

Kiumbe huvumilia, vikumbo na vijiwembe,
Ila siku hufikia, munkari umkumbe,
Ndipo watu hujalia wajapogeuzwa ng'ombe,
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

Hatimilki raia, aliye nayo atambe,
Wote tunao ubia, nchi yetu tuipambe,
Na karaha na udhia, usiwe wetu upambe,
Serikali ya kibabe, huangushwa na mibabe!

No comments: