Tuesday, November 15, 2011

Mkweli akiitwa mwongo

Ndivyo ilivyo dunia, waovu kusingizia,
Upofu watajitia, ukweli kutoujua,
Ni watu wa kuangamia, kwa dunia kutania,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Mrongo hujiumbua, uongo akiuzua,
Na kisha kumpakazia, msafi aliyekuwa,
Hata mkubwa akiwa, ni mtu wa kumzomea,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Laana waliovaa, ukweli huukataa,
Ili mradi wabwia, unga wa kukangamaa,
Lao kulipigania, japo laua raia,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Wapo wezi wa vifaa, na wapo wa watu pia,
Ila hawa ni balaa, wanaoiba sheria,
Na katiba kupindua, usafi wakajitia,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Na kisha kutangazia, umama kitu usojua,
Wanaharakati nia, na madhumuni mabaya,
Kuwa wamekusudia, umma kuupotoa,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Wote ninawaambia, mmeishiwa waheshimiwa,
Mkenge mmeingia, na watu hamjawajua,
Ya leo Tanzania, ya jana haitakuwa,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Umma mnaupindua, na katiba kuchakachua,
Na ukweli mnaujua, uchama mnatetea,
Nchi mwataka kugawa,kutawala kwendelea,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Tumeshawashtukia, na Mola twamgeukia,
Wape wasichotarajia, ewe wetu mkuu Alaa,
Juu zaidi ulokua, chini wapate ingia,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Wajua la kuwawia, na dua tunaitambua,
Usiku kuweka nia, na kisimamo kwingia,
Na masharifu na watawa, kufunga kwa hiyo nia,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Kwanza kuwachambua, kwa uongo kutwambia,
Na kisha kusingizia, ni warongo wasokua,
Dhambi kuwajazia, kibaba chao kujaa,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Fanya yao jumuia, Firauni ilokua,
Shamu wakishafkia, uje mwenyewe kuvua,
Na Mola mwenye kujua,ni haki utatumia,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

Afu twakutarajia, taifa kuliokoa,
Hao wanaojipendelea, ahera wangepigania,
Ili wapate tangulia, kama ukweli wajua,
Mkweli akiitwa mwongo, mrongo hujiumbua!!!

No comments: