Sunday, November 13, 2011

Usiwape tu walao

Tunawajua walao, na si wachapa kazi,
Hawa ni wajikombao, ujione ni Mwnye-enzi,
Ili wakipate chao, na walo kwao azizi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

Kati ya uwajuao, wajifanyao kipenzi,
Huujui moyo wao, na ndoto zao makazi,
Na hawa ndio wajao, kukufanyia ajizi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

Na ndio waonekanao, kuogopa uongozi,
Sio wafuasi wao, wala wasio na ngazi,
Na kazi waondoao,ni hawa kwenye mzizi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

Mengi moyo ufichao, si rahisi fumanizi,
Ni wachache wajuao, wengi hawayamaizi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

Watu uwachaguao, ukifanya utambuzi,
Ndio wakuangushao, ni chanzo pia mzizi,
Busara watumiao, huwa wajali ujuzi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

Hekima watumiao, huthamini ujuzi,
Na sio wapatanao, wala wa kwao wapenzi,
Kanuni hii ya cheo, kwa kila mwenye kuienzi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

Wengi waangukao, hutanguliza upenzi,
Wakasahau ya kwao, wajibu pia majenzi,
Na watu wayatakayo, halijengwi na ajizi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

Kati yetu tuombao, kuupata ufumbuzi,
Kila yajayo machweo, uwe wafanyia kazi,
Bora watu wafaao, nchi kuipa malezi,
Usiwape tu walao, wape na wafanyakzi!

No comments: