Thursday, November 24, 2011

Mwapenda msichoona?

Kaimu naishangaa, kupenda kisichokua,
Karibu kilichokua, kuacha kuangalia,
Fimbo ya mbali kuua, nyoka wasiyemjua,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

Ndani walioingia, wanazidi kuchukiwa,
Kama vile ndege hua, mwituni anayepaa,
Zaidi athaminiwa, si tunduini alokaa,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

Watu moyo huumia, kwa wanachokumbukia,
Na kile walichoshikilia, vigumu kuthaminiwa,
Na cha mbali huliliwa, cha ndani kuhujumiwa,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

Laiti wangelijua, tunaowahurumia,
Ubishi wanaozua, na talaka kulilia,
KIsa wanahadaiwa, na hao wapita njia,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

Pendo linalokufaa, si la ndoto kuotea,
Ni pendo lakushikilia, mikononi kulitia,
Kutomasa likakua, kila siku kuchanua,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

Bora ni ulichopewa, sio cha kutarajia,
Kile unachokilea, kikaja nawe kukufaa,
Kwingine kisikotulia, ila ulipokaa,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

Mengi twaangalia, kisha kuyafutulia,
Ku'delete' wanambia, neno wamelisanzua,
Moyo daima kutua, ukajenga mazoea,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

Na mnavyosimulia, kama vile mnalia,
Machoni kisichokuwa, kizuri sana kikawa,
Ila kikija jongea, hapo huwa ni balaa,
Mwapenda msichoona,pendeni mnachoona!

Wadudi namwinamia, mapenzi kuniridhia,
Nitosheke na dunia, zaidi kutolilia,
Niwe mwepesi kutoa, na mzito kupokea,
Mwapenda msichoona, pendeni mnachoona!

No comments: