Tuesday, November 15, 2011

Viziwi wa roho na moyo.

Ni heri ya kuzaliwa, kiziwi usiosikia,
Kuliko ya kuzaliwa, roho uliyepofua,
Hukuambaa dunia, ukadhani washikilia,
Viziwi si kwa sikio, ila kwa roho na moyo.

Roho isiposikia, mja huwa kafulia,
Viungo vingi huvia, moto vikiuhofia,
Hapana litalokua, vyote hujakusinyaa,
Viziwi si kwa sikio, ila kwa roho na moyo.

Moyo ukizuzuliwa, uwe usiosikia,
Huwa ni kubwa balaa, matamanio kukua,
Na iizidipo tamaa, hubaki kuangamia,
Viziwi si kwa sikio, ila kwa roho na moyo.

Na macho huyapofua, ishara kutozijua,
Zezeta nusu akawa, taahira kuzubaa,
Awe wa kuhurumia, mdomo anapofungua,
Viziwi si kwa sikio, ila kwa roho na moyo.

Moyo umenfiungua, wewe ulonichagua,
Haya ninafurahia, tena ninajivunia,
Na sifa kwako natoa, kingine sintochagua,
Viziwi si kwa sikio, ila kwa roho na moyo.

Si bora wa kuzaliwa, heshima wanipatia?
Kutosheka nimekua,na ukwasi sijajua?
Na milango wafungua,hata nisiyotarajia?
Viziwi si kwa sikio, ila kwa roho na moyo.

Naiombea Tanzania, viongozi kujaliwa,
Milki wanaojua, na ufalme usovia,
Hofu ikawaingia, na uongofu kuvaa,
Viziwi si kwa sikio, ila kwa roho na moyo.

No comments: