Wednesday, November 23, 2011

Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

VITA mnavyikimbia, waoga mmeshakua?
Mwawaje ni kina hawa, au mlituhadaa?
Kiume mlivyovaa, vingine kuwadhania?
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Katiba vita radhia, kila mtu kuingia,
Washairi mwatakiwa, mengi kuzungumzia,
Ili wapate kujua, hao wasiyoyajua,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Iliyopo kuzingatia, chimbuko la Tanzania,
Na mamlaka kujua,sasa nani atakua,
Naye kumpigania, hadi ukubwa kutwaa,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Na mkubwa twamjua, mwenyewe Mtanzania,
Si rais alokua, wala chama chake pia,
Ni mimi na wewe pia, ukuu tunaopewa,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Ni katiba yaamua, sio ninawaongopea,
Ila kinachotokea, katiba yapinduliwa,
Ukubwa wasiopwa, wataka kutuchezea,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Rais anatakiwa, hili kulizingatia,
Si mambo kujifanyia, kama kweli hajajua,
Na kisha kusingizia, waongo wasiokua,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Rais ni Mtanzania, hakuna wa kumzidia,
Ila katiba yakataa, juu ya wengine kua,
Kwenye kuiandaa, katiba yetu mpya,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Kusalimu kuamua, amri mmeshapewa,
Mzaha kwenu hatia, mashtaka mtazua,
Au mkajachukiwa, nchi kuingia makiwa,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Vyama vyote navyo sawa, hakuna kuteuliwa,
Chini kushuka murua, juu waliotangulia,
Tuzungumze raia, nchi tunayokusudia,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Ni heri kuzungumzia, tuliyoyakusudia,
Hata miezi ikiwa, mradi huru tukawa,
Tunakotoka kujua, na twendako kutambua,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Uzazi sio mzaha, wengi patashika hua,
Machungu kuvumilia, hadi mwana akazaliwa,
Na katiba kuizaa, ndivyo hivyo 'navyokua,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

Na katiba kuizaa, ndivyo hivyo 'navyokua,
Mwana kilema si dua, uzima twatarajia,
Na bora kilichokua, kiumbe kikitokea,
Mkowapi washairi, nchi kuipigania?

No comments: