Sunday, November 13, 2011

Abyadhi

Enzi zisizo na kadhi, mja huwa mwenye hasara,
Huikanyaga ardhi, hata bila ya tohara,
Akaikosa na radhi, ya huyo mwenye tijara,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

Nafsi huzibughudhi, akakosa maghufira,
Na baadhi na baadhi, huitaliki busara,
Haya yakawa maradhi,ya riha na masihara,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

Hata akipewa hadhi, anabakia majura,
Si mtu mwenye hafidhi,hukataa manusura,
Haithamini faradhi, na suna nazo hugura,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

Huna la kumkabidhi, ukaondokwa na ghera,
Manufaa hatokidhi, ila kwa yake bishara,
Na kuridhi hawaridhi, si mtu mwenye ashura,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

Moyoni yake kahodhi, ya shiriki na kafara,
Huona yake mahadhi, kwa kauli na sitara,
Husanii na lafudhi, umwone mwenye nusura,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

Dunia ina maudhi, haijapata shakira,
Haijawa mahfudhi, wala haifati dira,
Wala haijali hadhi, ni arijojo tiara,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

Hatambui abyadhi, ya Muhyi na ziara,
Humdhani ustadhi, mdowezi na fukara,
Hampi yake hifadhi, hata akipewa sura,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

Rabuka atupe radhi, waja wake mushtara,
Ya kwetu yote akidhi, pasiwe mwenye hasara,
Na kwake tujikabidhi, tuiepuke hasira,
Kama mtu abyadhi, sifuri sio duara!

No comments: